Siasa ya Wabunge Tanzania


Dar es Salaam. Ofisi ya Bunge jana ilitangaza
majina ya wenyeviti na makamu wapya wa
Kamati za Kudumu za Bunge huku Mbunge
wa Jimbo la Monduli, Edward Lowassa
akichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Kuchaguliwa kwa Lowassa kuongoza kamati
hiyo kunaibua upya vita kati yake na Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe, kutokana na wote
kutajwa kutaka kugombea urais katika
uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015.


Awali, Lowassa alikuwa Mwenyekiti wa
Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama,
ambayo iligawanywa hivi karibuni na
kuzaliwa kamati mbili; ya Ulinzi na Usalama
na Kamati ya Mambo ya Nje.
Kushinda kwa Lowassa kunakuja siku moja,
baada ya wabunge wote wa CCM kukutana
katika kikao cha ndani kilichofanyika Ukumbi
wa Karimjee na kujadili masuala mbalimbali,
ikiwa ni pamoja na jinsi ya kuwachagua
wenyeviti na makamu wa kamati hizo.
Habari za ndani kutoka katika kikao hicho
zilieleza kuwa moja ya ajenda
zilizozungumzwa ni kuwataka wabunge
kuwachagua wenyeviti kwa kufuata taratibu
na utendaji wao wa kazi.
Hata hivyo, Naibu Spika Job Ndugai aliliambia
Mwananchi Jumamosi kwamba kikao hicho ni
cha kawaida na walikuwa wakijadiliana
matatizo yaliyopo katika majimbo yao na jinsi
ya kuyawasilisha serikalini.
Katika uchaguzi huo, Musa Azzan Zungu
ambaye alikuwa makamu wa Lowassa kabla
ya kugawanya kwa kamati hiyo,
amechaguliwa tena kushika nafasi hiyo.
Uchaguzi wa wenyeviti na makamu wao
ulifanyika jana katika Ofisi Ndogo za Bunge
jijini Dar es Salaam, ikiwa ni siku moja baada
ya ofisi ya Bunge kutaja majina ya kamati
mpya 16 pamoja na wajumbe wake.
Uchaguzi huo umefanyika ukiwa umepita
mwezi mmoja tangu kumalizika kwa mkutano
wa 10 wa Bunge ambapo, Spika wa Bunge,
Anne Makinda alitangaza mabadiliko ya
kamati hizo, huku akiifuta Kamati ya Hesabu
za Mashirika ya Umma (POAC) iliyokuwa
ikiongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini,
Zitto Kabwe.
Kutokana na mabadiliko hayo, shughuli za
POAC sasa zitafanywa na Kamati ya Hesabu za
Serikali (PAC).
Kamati nyingine iliyofutwa ni ile ya Sheria
Ndogo wakati zimeundwa kamati mpya za
Bajeti, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
na ya Ulinzi na Usalama.
Taarifa za ndani kutoka katika chaguzi hizo
zinaeleza kuwa Zitto ambaye alikuwa
akichuana na John Cheyo, alipata kura 13 kati
ya 17 zilizopigwa na wajumbe wa kamati
yake, hivyo Zitto sasa ndiye Mwenyekiti wa
Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC).
Powered by Blogger.