Zuia UKIMWI timiza ahadi YAKO


Kifua Kikuu na Ukimwi ni miongoni mwa
magonjwa yaliyo kwenye orodha ya magonjwa
yanayoongoza kwa kuua watu wengi nchini.

Pamoja na ukweli huo, inawezekana
kupunguza kasi ya maambukizi, hata vifo
vinavyosababishwa na magonjwa hayo, ikiwa
jamii itashirikishwa moja kwa moja katika
mapambano dhidi ya magonjwa hayo.
Huu ni mtazamo wa Maria Francis ( 51),
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanaoishi na
Virusi vya Ukimwi (UWAVVU), chenye
maskani yake Kata ya Ilongero Wilaya ya
Singida, Mkoa wa Singida.
Mama huyu ambaye pia ni Katibu wa Chama
cha Waliowahi Kuugua Kifua Kikuu Ilongero,
amekuwa na mtazamo tofauti na watu wengi
kuhusu mapambano dhidi ya magonjwa hayo.
“Unaweza kushangaa ni kwa nini
ninapozungumzia Ukimwi nauunganisha na
Kifua Kikuu, lakini ukweli ni kwamba hii
inatokana na hali halisi kuwa magonjwa haya
hubebana,” anasema.
Kijiji cha Ilongero kinatajwa kuwa mfano
katika mapambano dhidi ya Kifua Kikuu na
Ukimwi kutokana na mipango yake kadhaa ya
kuanzisha vikundi vya uhamasishaji
mapambano dhidi ya magonjwa hayo.
Maria anasema kuwa baada ya kuona watu
wengi wanaona aibu kwenda kupata
matibabu, hata kupima wanapokuwa na
wasiwasi wa kuambukizwa ya maradhi hayo,
waliona ni vyema kutafuta mbinu mpya ya
kuwasaidia.
“Nikiwa mmoja wa watu walioathirika na
Ukimwi na Kifua Kikuu niliona ipo haja
kuwakusanya wenzangu tukaunda vikundi
kwa ajili ya kupambana na maradhi haya ili
kuinusuru jamii inayotuzunguka hasa watoto
wetu,” anasema Maria ambaye ni mama wa
watoto watatu.
Anaeleza kuwa walifanikiwa kuunganisha
nguvu na kuunda vikundi viwili, cha kwanza
kilikuwa cha wanaoishi na Virusi vya Ukimwi
na kile cha waliowahi kuugua Kifua Kikuu
huku kila kikundi kikiwa na malengo yake,
ingawa kazi zake zilifafnana.
Anabainisha kuwa kikundi cha wanaoishi na
Virusi vya Ukimwi kina kazi ya kuhamasisha
jamii kujenga utaratibu wa kupima afya.
“Kwa watakaoonekana kuathirika na kuanza
matibabu hupewa elimu juu ya matumizi
sahihi ya dawa na ulaji wa lishe bora,”
anasema Maria.
Anaongeza: “Mbali na elimu pia tumeanzisha
miradi ya maendeleo inayolenga kutuongezea
kipato na kuboresha afya zetu.”
Powered by Blogger.